Je, Tanzania iko tayari kwa umeme wa nyuklia?

Chanzo cha picha, MANTRA
- Author, Yusuph Mazimu
- Nafasi,
- Akiripoti kutoka BBC Dar es Salaam
"Ndani ya nchi yetu Mungu ametubariki uraniamu (urania). Ni vyema kusimamia ule mradi wetu kule Namtumbo, wale wawekezaji waanze kazi sasa tufaidike na rasilimali ile."
Ni kauli nzito ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa mwishoni mwa wiki wakati wa kumuapisha Mkurugenzi mtendaji mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange.
Kauli hiyo haikufichua tu msimamo wa kisera wa taifa, bali ilidhihirisha pia utashi wa juu wa kisiasa wa kuanza safari ya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa kutumia madini ya urani yanayopatikana nchini humo.
Mradi wa Mkuju River uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma ndiyo unatazamwa zaidi, lakini maeneo mengine kama Bahi, Galapo, Minjingu, Mbulu, Simanjiro, Ziwa Natron, Manyoni, Songea, Tunduru, Madaba, na Nachingwea nayo yamegundulika kuwa na madini haya muhimu.
Inakadiriwa kuwa Tanzania ina hifadhi ya takribani tani 58,500 za urani ambazo tayari zimethibitishwa, huku tafiti zaidi zikiendelea. Bila shaka, haya yote yanazidi kuimarisha matumaini kuwa urani inaweza kuwa msingi wa mabadiliko ya nishati nchini.
Lakini pamoja na nia hiyo dhahiri ya kisiasa, swali linabaki, Je, Tanzania iko tayari kwa teknolojia hii hatarishi lakini yenye manufaa makubwa?
Uranium ni nini, na umeme wa nyuklia unapatikanaje?

Chanzo cha picha, NAC
Urani ni madini ya asili yenye mionzi, na huwa na uwezo mkubwa wa kutoa joto kubwa kupitia mchakato wa nyuklia unaoitwa 'nuclear fission' yaani mgawanyiko wa atomu wa madini haya. Katika hatua hiyo, joto linalotolewa hutumika kuchemsha maji, na mvuke unaotoka husukuma mitambo ya 'turbine' inayozalisha umeme. Tofauti na njia za kawaida zinazotumia mafuta, gesi au makaa ya mawe, nishati ya nyuklia hutegemea nguvu ya ndani ya atomu.
Kwa sasa, zaidi ya mataifa 30 duniani yanatumia madini ya urani kuzalisha umeme. Kazakhstan inaongoza duniani kwa uzalishaji wa urani, ikifuatiwa na Australia, Namibia, Canada, Uzbekistan na Niger. Makampuni manane duniani yanadhibiti karibu asilimia 85 ya urani yote, huku Kazatomprom ya Kazakhstan ikiwa na hisa ya robo ya soko hilo.
Katika bara la Ulaya, Ufaransa huzalisha zaidi ya asilimia 70 ya umeme wake kupitia vinu vya nyuklia. Mataifa makubwa kama Marekani, China, Korea Kusini na hata Afrika Kusini yamepiga hatua kubwa katika teknolojia hii.
Kauli ya Rais Samia inasisitiza: "Umeme wa nyuklia kama wao wanautumia (nchi za Magharibi), tunaweza kuutumia, tukawa na umeme wa kutosha nchini na kuuza nchi jirani."
Mradi wa Mkuju River, Namtumbo ambao ulianza kuvutia wawekezaji miaka iliyopita kabla ya kusimama kwa muda, unaonekana sasa kupata uhai mpya. Serikali inaonyesha dhamira ya dhati ya kulifufua tena wazo hili, kwa kuweka mbele usalama na faida za kiuchumi zitokanazo na nishati hiyo.
Uranium ni tishio au fursa?

Chanzo cha picha, EPA.gov
Kama ilivyo kwa kila teknolojia yenye nguvu kubwa, nishati ya nyuklia inaibua maoni tofauti. Wapo wanaoiangalia kama nafasi na fursa adimu kwa Tanzania kujitegemea katika uzalishaji wa nishati ya ziada na kuachana na utegemezi wa umeme kutoka vyanzo vya mafuta na mabadiliko ya tabianchi.
Kundi hili linaamini, urani ni zawadi ya kimungu na rasilimali isiyopaswa kupuuzwa. Ni fursa muhimu ya kuimarisha uchumi. Ingawa Tanzania inazalisha umeme takribani Megawati 3500 kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya umeme, wakati mahitaji yake yakiwa chini ya Megawati 2000, ziada ya umeme ni kuihakikishia upatikanaji wa umeme kwenye shughuli za uzalishaji lakini pia inaweza kuuza nishati hiyo kwa majirani.
Lakini pia wapo wanaoona hatari ya rasilimali hiyo. Historia inaonyesha kwamba ajali kama ile ya Chernobyl nchini Ukraine mwaka 1986, na Fukushima nchini Japani mwaka 2011, ziliacha majeraha ya kudumu kwa mazingira, maisha ya watu, na afya za jamii. Madhara ya mionzi yake ina tabia ya kukaa kwa miongo mingi, mara nyingine hata zaidi ya karne.
Kwa ujumla mchakato wa uchimbaji wa urani nao si salama. Katika maeneo yenye urani karibu na uso wa ardhi, wachimbaji hutumia mbinu ya "open pit" ambayo huondoa kabisa udongo wa juu, jambo linaloharibu kabisa mazingira. Katika maeneo yenye urani ardhini kwa kina kirefu, wachimbaji hulazimika kuchimba migodi ya chini, na kisha kusafisha mawe ya urani kutoka kwenye miamba.
Baada ya uchimbaji, mabaki yenye mionzi huitwa tailings (taka imara), na yale ya kimiminika huitwa raffinates. Vyote vinaweza kusababisha uchafuzi mkubwa wa ardhi, maji na hewa.
Wataalam wa Tanzania wanaliona hili. ''Teknolojia ya nyukilia inaweza kuwa na madhara makubwa kwa binadamu kama haitatumiwa kwa usahihi',' anasema Profesa Lazaro Busagala, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Atomiki nchini Tanzania.
Kulingana na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC), urani hushambulia figo moja kwa moja, na kuleta madhara makubwa kiafya kwa binadamu na wanyama wanaoishi karibu na migodi au kunywa maji yaliyochafuliwa na mionzi. Uchafuzi wa maji ndiyo hofu kuu ya muda mrefu, kwani urani na mabaki yake huingia ardhini na kwenye vyanzo vya maji, hivyo kuathiri afya ya binadamu kupitia matumizi ya kila siku.

Chanzo cha picha, IAEA
Mtaalamu kutoka Ujerumani, Gunter Wippel ambaye ni mwenyekiti wa Shirika la Uranium Network, aliwahi kuishauri Tanzania kuachana na uchimbaji wa madini haya kwa kuzingatia madhara yake. Naye Profesa Andreas Nidecker kutoka Mtandao wa Kimataifa wa madaktari dhidi ya vita vya nyuklia (IPPNW) alinukuliwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa akisema: "Watu katika mataifa ambayo huzalisha kwa wingi urani wamekumbana na matatizo zaidi kuliko faida za kiuchumi. Tatizo la hivi karibuni la Yokoshima limedhibitisha kitisho kilichoko kwenye matumizi ya nyuklia."
Mashirika ya mazingira duniani pia yanaonya kuwa hata uchimbaji wa urani pekee unaweza kuharibu vyanzo vya maji, kuathiri kilimo, na kusababisha magonjwa ya saratani katika jamii. Katika nchi kama Tanzania ambayo ndiyo inajenga mfumo imara wa ufuatiliaji wa afya na mazingira, hoja hizi si za kubezwa.
Je, Tanzania iko tayari?

Chanzo cha picha, mantra
Kisiasa, Tanzania inaonekana ipo tayari. Dola zaidi ya bilioni moja tayari zimewekezwa katika mradi wa Mkuju, na miradi mingine iliyo katika hatua za mwanzo, jambo linaloifanya nchi kuwa miongoni mwa mataifa matano ya Afrika yaliyo kwenye harakati za juu za uzalishaji wa urani. Lakini kuzalisha umeme wa nyuklia si suala la kuamuliwa tu kisiasa. Ni safari ndefu inayoihitaji nchi kuwa tayari kielimu, kisheria, kiteknolojia na kimazingira.
Kwa upande wa sheria na taasisi, Tanzania ina Sheria ya Nguvu za Atomiki ya mwaka 2003, ambayo iliunda Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC). Hii ni hatua muhimu kwa usimamizi wa shughuli zote zinazohusu mionzi na teknolojia ya nyuklia.
Katika sekta ya elimu, wataalamu waliobobea katika fizikia ya nyuklia, kemia, uhandisi, usalama wa mionzi na hata sheria za kimataifa kuhusu nyuklia wanahitajika wa kutosha. Bila wataalamu hawa, hata uwekezaji mkubwa hautaweza kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Ingawa Tanzania haijakiri uchache wa wataalam wa aina hii, kwa ujumla Afrika inakabiliwa na uhaba wa wataalam hawa.
Profesa Busagala, Mkurugenzi TAEC, amefichua kuwa mpango wa Tume hiyo kudhamini vijana watano wa Kitanzania kila mwaka ili kusomea teknolojia ya nyuklia.
Akieleza mipango ya TAEC, Profesa Busagala alisema: "Kufuatia mpango wa mafunzo ulioanza kutekelezwa, TAEC tayari imetoa mafunzo kwa watumishi wake 29 na inaendelea kudhamini wengine 32 ndani ya kipindi cha miaka mitatu, jambo linalofanya jumla ya watumishi wa umma 61 kunufaika."

Chanzo cha picha, URT
Ukiacha elimu, Mitambo ya nyuklia inahitaji si tu majengo ya kisasa, bali pia mifumo ya kusafisha na kuhifadhi taka za mionzi kwa mamia ya miaka. Uwekezaji wa muda mrefu wa kiusalama, kisheria, na kiufundi ili kufanikisha ndoto hii ni muhimu.
Mwalimu wa fizikia kutoka Tabora, Rahman John, anasema: "Kama Tanzania imeweza kuanza na uwekezaji wa dola bilioni 1 kule Namtumbo na kwingineko, imewekeza mabilioni ya dola kwenye mradi wa umeme wa Bwawa la Nyerere (JNHPP), sioni ikishindwa kwenye nyuklia, kama Rais mwenyewe ameonyesha nia na utashi wake."
Kweye hoja ya usalama na madhara yake, Chris Sattler, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Uranium One Inc inayosimamia mradi wa Mkuju kupitia kampuni tanzu ya Mantra Tanzania, anasisitiza kuwa: "Kama ilivyo kwa miradi mingine ya urani, mradi huu wa Mkuju utazingatia taratibu zote za kiusalama za kitaifa na kimataifa."
Tanzania imeanza safari ya nishati ya nyuklia kwa misingi mizuri ya dhamira ya kisiasa na rasilimali ya kutosha. Hata hivyo, mafanikio ya safari hii yatategemea zaidi namna ambavyo nchi itajipanga kitaasisi, kielimu, na kiteknolojia. Uranium inaweza kuwa tumaini kubwa la kiuchumi kwa Tanzania, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha majanga ikiwa haitasimamiwa kwa makini.
Mjadala zaidi utaendelea kwenye eneo la uwezo wa kudhibiti teknolojia hii kwa usalama wa vizazi vijavyo. Kwa sasa, Tanzania inaonekana kujiandaa. Lakini bado ipo haja ya kujifunza, kujipanga, na kushirikiana na mataifa mengine ili kuhakikisha kuwa inapiga hatua salama kuelekea umeme wa nyuklia.