Fahamu vita vya nyuklia vilivyoitikisa dunia

Asha Juma

BBC Swahili

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mawingu ya muundo wa uyoga ya bomu la nyuklia juu ya anga la Hiroshima (kushoto) na Nagasaki (kulia)

India na Pakistan majirani wenye silaha za nyuklia wanaendela kupigana katika vita vilivyoshuhudiwa katika maeneo ya nchi zote mbili. Dunia inawasiwasi na matumizi ya siala hizi.

Mvutano huu ni sehemu ya mzozo ambao umedumu kwa muda mrefu, chimbuko lake likiwa India na Pakistan zote kudai udhibiti wa eneo lote la Kashmir.

Wakati wa vita hivyo, tayari dunia ilikuwa imeanza kuingia kiwewe hasa ikizingatiwa kuwa nchi zote zina silaha za nyuklia, jambo ambalo lilisababisha Marekani na nchi zingine kama vile Saudi Arabia, Iran, UAE na Uingereza kuingilia kati ili kushinikiza upatikanaji wa suluhu kwa njia ya kidipomasia.

Lakini mbona mzozo kati ya majirani hawa uitie dunia wasiwasi?

Vita vya nyuklia kuwahi kutokea duniani

Soma zaidi:

Hadi kufikia sasa, silaha za nyuklia zimetumiwa mara moja tu katika mapigano ya kijeshi mwaka wa 1945 wakati Marekani ilipodondosha mabomu ya nyuklia huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japani na madhara yake ni jambo ambalo halitawahi kusahaulika milele.

Wakati Japani inavamiwa na Marekani, vita vya pili vya dunia vilikuwa vimeisha, na Ujerumani tayari ilikuwa imesalimu amri mnamo mwezi Mei mwaka 1945.

Lakini kumbe, vita vilikuwa vinaendelea katika eneo la Pasifiki, na Japani ilikuwa imevamia sehemu nyingi za Asia ambazo zilikuwa zimetawaliwa na jeshi lake, kama vile Korea, kaskazini ya China, Indonesia, Vietnam na nyinginezo.

Kile ambacho walikuwa hawafamu ni kwamba majeshi ya Marekani yalikuwa yamepiga hatua taratibu kuikabili Japani.

Jaribio la kwanza la bomu la nyuklia lilifanyika katika jangwa la New Mexico, mnamo Julai 16, 1945, na aliyekuwa Rais wa Marekani Harry Truman, alikuwa tayari ameidhinisha matumizi yake dhidi ya Japani kwa matumaini ya kumaliza vita.

Ikumbukwe kwamba Japani ilifanya shambulizi la kushtukiza dhidi ya Marekani mnamo Desemba 7, 1941, kwenye kambi ya jeshi ya Marekani katika Bandari ya Pearl, Hawaii.

Shambulio hilo lilisababisha uharibifu mkubwa kwa meli ya Pasifiki ya Marekani, na pia vifo wanajeshi zaidi ya 2,400 wa Marekani na raia.

Shambulizi hilo lilichochea Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia.

Siku moja baada ya shambulio hilo, Rais Franklin D. Roosevelt alitaka Bunge kutangaza vita dhidi ya Japani.

Kando na mashambulizi ya Hiroshima na Nagasaki, Japani ilipata shinikizo kubwa baada ya Umoja wa Soviet kutangaza vita rasmi mnamo Agosti 8.

Mnamo 6 Agosti 1945, Marekani ilidondosha bomu la nyuklia lililotengenezwa kwa madini ya urani katika mji wa viwandani wa Hiroshima na papo hapo mamia ya watu walipoteza maisha kutokana na mionzi.

Siku tatu baadaye, Marekani ilidondosha bomu jingine la nyuklia huko Nagasaki.

Na hilo likawa chanzo cha Japani kijisalimisha, na kumaliza Vita vya Pili vya Dunia.

August 15, 1945, Mfalme Hirohito wa Japani, sauti yake ilisikika kupitia radio akisema kuwa sasa nchi hiyo imesalimu amri kwa sababu ya mashambulizi ya bomu yaliodondoshwa Hiroshima na Nagasaki.

Chimbuko la bomu lililodondoshwa Hiroshima and Nagasaki

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mji wa Hiroshima ulioharibiwa baada ya mlipuko wa bomu la nyuklia

Ugunduzi wa kiini cha atomu cha nyuklia mwaka 1938 uliwezesha hatua kupigwa na kuongeza uwezekano wa kutengenezwa kwa bomu la nyuklia kinadharia.

Awali, kulikuwa na hofu kwamba mradi wa bomu la nyuklia wa Ujerumani utaendeleza silaha za nyuklia.

Hii ilichochea kuanza kwa utafiti wa awali nchini Marekani mwishoni mwa 1939. Maendeleo yake yalikuwa polepole hadi kulipotokea ripoti iliyoonyesha kuwa kilo 5 hadi 10 tu za madini halisi ya uranium-235 zilihitajika kutengeneza bomu.

Na mradi wa kuanza utengenezaji wa bomu ukaanza rasmi.

Kulikuwa na programu ya silaha za nyuklia ya Japani, lakini haikuwa na rasilimali za kibinadamu, madini wala fedha, hivyo basi, hakukuwa na maendeleo mengi kuelekea kutengeneza bomu la nyuklia.

Bomu la "Little Boy" - Hiroshima - Agosti 6, 1945

Bomu la nyuklia lililotumiwa huko Hiroshima, Japani, Agosti 6, 1945, lilipewa jina la "Little Boy".

Bomu hilo lilidondoshwa na ndege ya Marekani ya B-29 inayoitwa Enola Gay, iliyoanza safari kutoka kisiwa cha Tinian kuelekea Japani.

Eneo lengwa la shambulizi hilo lilikuwa jiji la Hiroshima, lililoko kwenye delta za kusini-magharibi mwa Kisiwa cha Honshu kando ya Bahari ya Kati.

Silaha hiyo ya aina ya bunduki ilikuwa na nguvu ya pauni 9,700 ya madini ya urani.

Bomu la "Little Boy" lilidondoshwa saa mbili na dakika 15 asubuhi Agosti 6, 1945, kulingana na Jeshi la Majini la Marekani, kwa urefu wa futi 1,800 juu ya mji wa Hiroshima.

Kanali Tibbet, ambaye ndiye alikuwa anadondosha bomu hilo, alifanya hivyo kwa haraka sana kuepuka mitikiso iliyokuwa inatarajiwa.

Sekunde arobaini na tatu baadaye, mlipuko mkubwa uliwaka kwenye anga wakati bomu la "Little Boy" linalipuka, moja kwa moja kwenye uwanja ambapo wanajeshi wa Jeshi la Pili la Japani walikuwa likifanya mazoezi ya mwili.

Ingawa tayari ndege ya Enola Gay ilikuwa umbali wa maili kumi na moja na nusu, ilitikiswa na mlipuko huo.

Idadi ya vifo iliyorekodiwa ni makadirio tu, lakini inadhaniwa kuwa karibu 140,000 ya idadi ya watu 350,000 wa Hiroshima jiji la kiviwanda, waliuawa katika mlipuko huo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waliokuwepo kwenye ndege ya Enola Gay, ambayo ilidondosha bomu la nyuklia katika jiji la Hiroshima

Bomu la "Fat Man" - Agosti 6, 1945

Mbali na bomu la kwanza, Japani ilishambuliwa tena kwa bomu la pili, siku tatu tu baadaye, lililokuwa limepewa jina la "Fat Man".

Bomu hili lilikuwa na vilipuzi upande wa nje ambao ungelipuka na kusababisha mitikiso na mlipuko wa nyuklia.

Kwa sababu tayari idhini ya kufanya mashambulizi ya nyuklia ilikuwa imetolewa kitambo, kilichosalia ilikuwa tu suala la utekelezaji na saa tisa na dakika 47 alfajiri, Agosti 9, 1945, ndege ya B-29 kwa jina Bock's Car iliondoka kisiwa cha Tinian ikielekea eneo la kutengenezea silaha la Kokura Arsenal.

Hali ya hewa ilikuwa imeripotiwa kuwa ya kuridhisha mapema siku hiyo lakini wakati B-29 inawasili, ilikuwa imebadilika.

Kulikuwa na moshi na ukungu hivyo basi, ikawa vigumu kwao kuona eneo lengwa.

Kokura haikuonekana tena kuwa chaguo muafaka, na kulikuwa na mafuta ya kutosha tu kurudi kwenye uwanja wa pili wa ndege Okinawa, kukafanywa maamuzi ya kuondoka hapo na kuelekea eneo lengwa la pili, Nagasaki.

Hali ya hewa huko nako pia haikuwa nzuri, lakini dakika za mwisho, rubani alifanikiwa kuona uwanja wa jiji la Nagasaki.

Saa 11:02 asubuhi, kwenye mwinuko wa mita 1,650, bomu la "Fat Man" lilidondoshwa.

Nagasaki ilikuwa kituo cha viwanda na bandari kubwa kwenye pwani ya magharibi ya Kyushu.

Bado kulikuwa na watu karibu 200,000 katika jiji hilo wakati bomu linalipuka na inakadiriwa kuwa takriban 74,000 walifariki dunia.

Mabomu hayo ndio yalichochea kumalizika kwa vita huko Asia, na Japan ikijisalimisha kwa washirika wake.

Madhara ya bomu la nyuklia

Wale ambao walinusurika mabomu ya Hiroshima na Nagasaki wanajulikana kama Hibakusha.

Waathirika walikabiliwa na athari mbaya katika miji, pamoja na sumu ya mionzi na kiwewe cha kisaikolojia.

Tahadhari: Simulizi hizi huenda zikakuumiza moyo

Emiko alikuwa na umri wa miaka minane wakati bomu la nyuklia lilipodondoshwa huko Hiroshima.

Dada yake mkubwa, Mieko, na jamaa wao wengine wanne waliuawa.

.

Chanzo cha picha, Courtesy of Emiko Okada

Maelezo ya picha, Emiko akiwa mikononi mwa mama yake Fuku Nakasako, na dada yake Mieko

"Dada yangu aliondoka nyumbani asubuhi hiyo, akisema, 'Tutaonana baadaye!' Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili tu na mchangamfu sana," alisema Emiko.

"Lakini hakurudi tena. Hakuna anayejua kilichompata.

"Wazazi wangu walimtafuta sana wakiwa na matumaini labda pengine wataona mwili wake, hivyo waliendelea kusema kwamba lazima yuko hai.

"Mama yangu alikuwa mjamzito wakati huo, ila mimba iliharibika.

"Hatukuwa na chochote cha kula. Hatukujua kuhusu mionzi, kwa hivyo tuliokota chochote tulichoweza kupata bila kufikiria ikiwa kilikuwa na mionzi au la.

"Kisha nywele zangu zilianza kunyonyoka, na fizi zangu zikaanza kuvuja damu. Nilikuwa ninachoka kila mara nakulazimika kulala chini kila wakati.

"Hakuna mtu wakati huo alikuwa anafikiria kuhusu mionzi. Miaka kumi na miwili baadaye, niligunduliwa kuwa na 'aplastic anaemia' – tatizo nadra sana la damu lakini baya kwa sababu uboho wa mfupa unashindwa kutengeneza seli mpya za damu, na kusababisha upungufu katika seli nyekundu, nyeupe, na vigandishadamu.

Reiko Hada

.

Chanzo cha picha, Lee Karen Stow

Reiko Hada alikuwa na umri wa miaka tisa wakati bomu la atomiki liliporushwa kwenye mji wake wa nyumbani wa Nagasaki saa tano na dakika mbili asubuhi mnamo 9 Agosti, 1945.

Mapema asubuhi hiyo, ving'ora vilisikiksa kuashiria onyo la kushambuliwa kwa ndege, kwa hiyo, Reiko akabaki nyumbani.

Baada ya ving'ora kutulia, alikwenda kwenye hekalu la karibu, ambapo watoto katika kitongoji chake walikuwa wakisoma huko wakati hawaendi shule, kwa sababu ya maonyo ya mara kwa mara ya uvamizi wa anga.

Baada ya dakika 40 hivi za kusoma kwenye hekalu, walimu waliwaruhusu kwenda nyumbani.

"Nilifika kwenye mlango wa nyumba yetu, na nadhani nilipiga hatua kuingia ndani," Reiko alielezea BBC.

"Kisha ghafla. Mwanga mkali uliangaza machoni mwangu. Rangi zilikuwa za manjano, khaki na machungwa, zote zikiwa zimechanganyikana.

"Sikuwa na wakati hata wakufikiria ilikuwa nini... Muda si muda, kila kitu kiligeuka kuwa cheupe kabisa.

"…kidogo nikasikia kishindo kikubwa. Kisha sikujua kilichokuwa kikiendelea.

"Baada ya muda, nikamtafuta mama yangu, tukatoka kwenda kwenye eneo salama.

.

Chanzo cha picha, Courtesy of Reiko Hada

"Sikujua kuwa nimeponea kifo chupuchupu. Lakini upande wa pili wa mlima; hali ilikuwa mbaya.

"Watu wengi walikuwa wanakimbia kuja upande tuliokuwa wa chuoni. Macho yao hayakuwa kawaida, yalikuwa yametoka nje, nywele zao zimechanika, karibu wote walikuwa uchi, walikuwa wameungua vibaya na ngozi zao zinaning'inia.

"Mama yangu na wengine walikimbilia kuchukua taulo na shuka majumbani na kuanza kuwaongoza watu waliokuwa wakija eneo salama ambapo wangeweza kulala.

"Waliomba maji, na nikapewa jukumu la kutafuta bakuli, na kwenda mto jirani kuchota maji ili wanywe.

"Baada ya kunywa maji kidogo tu walifariki dunia, watu walianza kufa mmoja baada ya mwingine.

"Ilikuwa majira ya joto. Kwa sababu ya funza na harufu mbaya, miili ililazimika kuchomwa mara moja. Ilirundikwa kwenye bwawa la kuogelea chuoni hapo na kuchomwa kwa kuni chakavu.

"Ilikuwa vigumu kutambua ni akina nani. Hawakufa kama wanadamu".

"Natumai vizazi vijavyo havitawahi kupitia hili. Hatupaswi kamwe kuruhusu [silaha hizi za nyuklia] kutumika.

"Ni watu wanaohakikisha uwepo wa amani. Hata kama tunaishi katika nchi tofauti na kuzungumza lugha tofauti, matakwa yetu ya amani ni sawa."

Hatari ya vita vya nyuklia kati ya India na Pakistan ni ya kweli kiasi gani?

Kwa mifumo mipya ya uwasilishaji na maendeleo ya kiteknolojia, vinu vinne vya plutonium na kuongezeka kwa urutubishaji wa madini ya uranium, silaha za nyuklia za Pakistan zinaweza kufikia karibu makomnora ya nyuklia 200 kufikia mwishoni mwa miaka ya 2020, kulingana na The Nuclear Notebook , iliyotafitiwa na Shirikisho la Mradi wa Taarifa za Nyuklia za Wanasayansi wa Marekani.

Na mwanzoni mwa 2023, India ilikadiriwa kuwa na takriban kilo 680 za plutonium ya kiwango cha silaha - ya kutosha kwa takriban makombora ya nyuklia 130-210, kulingana na Jopo la Kimataifa la Fissile Materials.

Licha ya migogoro ya mara kwa mara kati ya Pakistan na India, kwa uingiliaji kati wa haraka na nchi za nje, pande zote mbili hadi sasa zimefanikiwa kuzuia janga la mzozo wa nyuklia.

Lakini swali ni je, wataweza kujizuia hadi lini?

"Wakati ambapo silaha za nyuklia zinaweza kutumia, daima kuna kiwango cha hatari kisichokubalika," John Erath, mkurugenzi mkuu wa sera katika Kituo cha Kudhibiti Silaha na Kuzuia Kueneza Silaha, aliambia BBC.

"Serikali za India na Pakistan zimepitia hali hizi hapo awali, hivyo hatari ni ndogo. Lakini palipo na silaha za nyuklia, hata hatari ndogo ni kubwa mno."