Wanaharakati maarufu wanaozikosesha usingizi nchi zao Afrika Mashariki

.

Chanzo cha picha, Reuters

  • Author, Abdalla Seif Dzungu
  • Nafasi, BBC Swahili
  • Twitter,
  • Akiripoti kutoka Nairobi Kenya

Askofu mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Benson Bagonza anatafsiri uanaharakati kama imani na ushawishi katika jambo fulani analosimamia mtu na kulipigania.

Uanaharakati ni neno la kiarabu lenye maana ya mchakato wa mtu ama watu kufuatilia jambo fulani wanaloamini lina maana ama la msingi kwa maisha ya jamii.

Na kwa nchi nyingi hasa za Kiafrika watu hawa huonekana kama maadui wa mamlaka na wakati mwingine hupitia maisha na wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yao na kufikia malengo yao.

Ifuatayo ni orodha ya wanaharakati ambao wanaonekana mwiba kwa mataifa yao Afrika Mashariki.

Pia unaweza kusoma

Maria Sarungi - Tanzania

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi Tsehai

Ni mwanaharakati aliyejikita zaidi kwenye kutaka mabadiliko akitumia mitandao ya kijamii zaidi kutekeleza azma yake hiyo.

Kampeni iliyompa umaarufu zaidi ni "Change Tanzania" iliyoanza kama hashTag kwenye mtandao wa Twitter, na kwa sasa amekuwa akiendesha mijadala mikubwa inayohusisha maelfu ya Watanzania kupitia jukwaa la "Space" la Twitter.

Mijadala hii kwa kiasi kikubwa inakosoa mamlaka kwenye maeneo mbalimbali, lakini pia inachochea ushawishi wa masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya katiba ya nchi, kuondolewa kwa sheria kandamizi na kuchochea uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

Maria amekuwa akiendesha shindano la urembo la Miss Universe Tanzania akiwa ni mtaalam wa mawasiliano na uandishi wa habari, na mmiliki wa kampuni ya Com communication.

Amekua akisimamia midahalo mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi kupitia kampuni yake.

Kupitia juhudi na uanaharakati wake aliteuliwa na aliyekuwa rais wa Tanzania wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa bunge la katiba mwaka 2014.

Kituo chake cha Kwanza TV kimekumbana na rungu la kufungiwa kutokana na maudhui yake yaliyoonekana kwenda kinyume cha sheria, Mijadala anayoiendesha na jumbe zake hasa kwenye mtandao wa twitter zimekuwa homa kali kwa mamlaka.

Hivi majuzi mwanaharakati huyu ambaye alikimbilia Kenya, na sasa anaishi katika taifa hilo la Afrika mashariki alinusurika jaribio la utekaji jijini nairobi.

Akizungumza na vyambo vya habari jijini Nairobi siku moja baada ya kuachiwa alisema watekaji hao walimuuliza ikiwa anahofia kuvushwa upande wa pili wa mpaka.

''Naamini kuwa Mtanzania alihusika. Sioni kwa nini Serikali ya Kenya iwe na nia kuniteka na kujaribu kuchukua simu zangu.''alisema.

Maria Sarungi ni mkosoaji mkubwa wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, na ameishutumu serikali yake kwa kurudisha "udhalimu" nchini humo.

Boniface Mwangi - Kenya

.

Chanzo cha picha, Getty Images/AFP

Maelezo ya picha, Mwanaharakati Boniface Mwangi

Boniface Mwangi aliacha uandishi wa habari baada ya kushuhudia na kupiga picha ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka wa 2007 kama mpiga picha wa magazeti.

Alipata mfadhaiko wa kiakili baada ya kuathiriwa moja kwa moja wakati watu wa jamii yake walipotishiwa

Aliathirika zaidi baada ya kulazimika kuwaangazia wanasiasa walewale waliochochea ghasia bila kuadhibiwa.

Mpango wake wa kwanza ulikuwa mradi wa Picha Mtaani, kwa Kiswahili "picha mtaani", ukionyesha picha za ghasia za mwaka 2007 baada ya uchaguzi wa kitaifa, kati ya makabila mbalimbali.

Maonyesho haya ya mitaani yalionyeshwa kote nchini kwa watu kujadili upatanisho.

Mwangi alikamatwa na polisi mwezi Mei 2019 kwa madai ya kuandaa mapinduzi nchini Kenya

Maafisa wa upelelezi walikuwa wamemkamata Bw Mwangi nyumbani kwake na kumpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako alirekodi taarifa.

Aliachiliwa muda mfupi baada ya taarifa inayoelezea mashtaka ambayo huenda akakabiliwa nayo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwaka 2024 Kuzuiliwa kwake kulikuja baada ya kuitisha maandamano dhidi ya serikali katika mbio za marathon katika mji mkuu, Nairobi.

Polisi walikuwa wamethibitisha kuwa Bw Mwangi alikuwa kizuizini lakini hawakutoa maelezo zaidi.

Kuzuiliwa kwake kulizua hasira miongoni mwa wafuasi wake, waliotaka aachiliwe.

Hivi karibuni , Mwanaharakati huyo aliachiliwa nchini Tanzania baada ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa siku tatu alipokuwa ameenda kuhudhuria kesi ya kiongozi wa chama cha upinzani Chadema.

Mwangi ambaye alishindwa kutembea baada ya kuachiliwa anasema aliteswa na kufanyiwa mambo mabaya wakati alipokuwa kizuizini nchini Tanzania.

Agather Atuhaire - Uganda

.

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha, Agather Atuhaire

Agather Atuhaire ni mwanasheria mashuhuri na mwanahabari mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 11.

Uandishi wake wa habari unazingatia michakato ya bunge, demokrasia ya vyama vingi, na mafuta na gesi.

Amechangia katika vyombo vya habari kama vile gazeti la Independent, Daily Monitor, Uganda Radio Network, BBC, na National Geographic.

Agather huonekana mara kwa mara kwenye vipindi vya mazungumzo vya NTV na NBS TV na amekuwa akiandaa kipindi kwenye Civic Space TV.

Akiwa na wafuasi wengi kwenye mtandao wa X, anajulikana kwa kuripoti kwake kwa matokeo kuhusu utawala na uwajibikaji.

Kazi ya Agather imemtambulisha kama sauti inayoaminika kuhusu utawala na haki ya kijamii nchini Uganda. Ameongoza sababu muhimu za haki za kijamii na Kampeni.

Hivi majuzi mwanaharakati huyo mashuhuri alikamatwa na kuzuiliwa kwa siku tatu nchini Tanzania pamoja na mwenzake wa Kenya Boniface Mwangi.

Atuhaire alikuwa amesafiri hadi Tanzania pamoja na mwanaharakati wa kupinga ufisadi nchini Kenya Boniface Mwangi kumuunga mkono kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, ambaye alifikishwa mahakamani Jumatatu.

Okiya Omtata kutoka Kenya

.

Chanzo cha picha, Okia Omtata/X

Maelezo ya picha, Okia Omtata

Huyu ni mwanaharakati kutoka nchini Kenya aliye mstari wa mbele kupinga maamuzi yoyote yanayokwenda kinyume na katiba ya nchi.

Licha ya kuwa Seneta wa kaunti ya Busia, Okia Omtata huenda akawa ndiye mwanaharakati aliyefungua kesi nyingi zaidi nchini Kenya dhidi ya masuala yanayokwenda kinyume na katiba, na si aghalabu siku moja kumkuta kwenye rekodi za kitabu cha Guinness kwa mtu aliyefungua kesi nying zaidi.

Okiya alizaliwa katika kaunti ya Busia November 30, 1964, na kujiunga na shule ya upili ya st Paul na huko akakutana na mchungaji ambaye ndiye aliyemshawishi kuwa alivyo leo.

Kabla ya kujiunga na shule ya Sekondari mtakatifu Peters School huko Mukumu alipomaliza elimu ya juu ya sekondari mwaka 1983.

"Uanaharakati nilianza nikiwa Sekondari ingawa nilikuwa mtiifu na mwenye heshima lakini nilikuwa nahoji sana, na ni wakati huo nilipoanza kuona umuhimu wa uhuru wa kujieleza".

Stella Nyanzi - Uganda

.

Chanzo cha picha, SUMY SADURNI

Maelezo ya picha, Stella Nyanzi

Ni msomi wa elimu ya juu na Profesa asiyeogopa kusema lolote analoamini tena wakati wowote hata kama linamuhusu Rais wa nchi.

Amekaa jela mara kadhaa kwa harakati zake dhidi ya mamlaka za Uganda. Alikuwa na kesi ya kumtukana Rais Museveni.

Alikaa jela kwa miezi 18 lakini kama haikutosha alipotoka tu akasema

"Museven lazima uondoke, nakupa notisi, uondoke, unaweza kufanya lolote tuko tayari, tumechoka, Museven, acha kukandamiza Waganda".

Aliwahi pia kukaa jela kwa siku 33 kwa kuchapisha kwenye mtandao wake wa Facebook ujumbe unaodaiwa kumtusi Rais Museveni.

Akiwa jela aliandika ushairi matata ambao ulisambaa na kukimbiliwa na wengi kutokana na maudhui yake ya kiuanaharakati.

Alitorokea Kenya kunusuru maisha yake, baada ya kuvamiwa na kuteswa na watu wanaoonekana kutokubaliana na matendo yake.