Koletha Kakuru: 'Nilijisaidia haja kubwa kupitia njia ya haja ndogo"

nn
Maelezo ya picha, Koletha Kakuru

Waswahili walisema hujafa hujaumbika. Usemi huo wa busara ya Kiswahili ulidhihirika mnamo mwaka 2019 kwenye Maisha ya Koletha, ambaye alikuwa na umri wa miaka 20 tu, yalibadilika kabisa baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza. Kwa bahati mbaya, wiki moja tu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, alianza kushuhudia mabadiliko yasiyo ya kawaida katika mwili wake – alianza kujisaidia haja kubwa kupitia njia ya haja ndogo, hali iliyomshtua sana.

Fuatilia Makala hii kwa kina iliyoandaliwa na Hilder Ngatunga wa BBC Media Action.

"Nilishtuka sana. Hata ndugu zangu walishangaa, hawakuwa wamewahi kuona tatizo kama hili," anasema Koletha kwa huzuni.

Kabla hata ya kupata jibu la matatizo hayo kiafya, alikumbana na tuhuma na maswali kutoka kwa mama yake ambaye alidhani huenda tatizo hilo limesababishwa na kufanya mapenzi akiwa bado mdogo au kufanya kazi ngumu akiwa na umri mdogo. Kauli hizo zilimvunja moyo zaidi na kuongeza msongo wa mawazo.

Wakati hali hiyo ikiendelea kuzidi kuwa mbaya, alijikuta akitengwa na familia na jamii. "Awali walikula pamoja nami, lakini baadaye wakaanza kuniepuka. Wifi yangu alikuwa anafunga mlango wa chumba chake ili nisiingie na kuacha harufu. Hata wageni wakija, alihakikisha sipo karibu nao," anasimulia kwa uchungu Koletha.

Skip Iliyosomwa zaidi and continue reading
Iliyosomwa zaidi