Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi aachiwa huru Tanzania

Chanzo cha picha, Haki Afrika
Mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi ameachiliwa huru na Tanzania, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki Afrika aliiambia BBC.
Hussein Khalid alithibitisha kuwa alikuwa pamoja na Mwangi wakiwa njiani kutoka Mombasa na sasa wanaelekea Nairobi.
Waziri Mkuu na Katibu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, awali alikuwa pia ametangaza kuachiliwa kwa mwanaharakati huyo karibu na eneo la mpaka kati ya nchi hizo mbili ambaye alikuwa amekamatwa nchini Tanzania kwa siku kadhaa.
Mudavadi, katika taarifa yake, alisema Mwangi aliachiliwa huru Alhamisi asubuhi na mamlaka ya Tanzania baada ya serikali kuingilia kati.
Hata hivyo, hakuna taarifa zozote zilizotolewa kuhusu hali yake ya afya hadi kufikia sasa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Awali, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Kenya ilisema kuwa "licha ya maombi kadhaa ya kumuona mwanaharakati huyo, maafisa wa Serikali ya Kenya hawakuwezeshwa kumfikia wala kuwa na habari zozote kumhusu Bw Mwangi."
Wizara hiyo pia ilionyesha wasiwasi juu ya afya yake na kukosekana kwa habari kuhusu kuzuiliwa kwake," ilisema.
Kenya ilitoa wito kwa serikali ya Tanzania kuchukua hatua ya "haraka na bila kuchelewa" ili kuwezesha ufikiwaji wa kibalozi au kuachiliwa kwa Mwangi, kwa mujibu wa sheria na kanuni za kimataifa kidiplomasia.
Mwanaharakati Boniface Mwangi na Agather Atuhaire wa Uganda walizuiliwa nchini Tanzania mapema wiki hii nchini Tanzania, ambao walikuwa wameenda kuhudhuria kesi ya kiongozi wa CHADEMA Tundu Lissu.

Hapo jana, Njeri Mwangi, mkewe Boniface Mwangi aliandamana na mwanawe mkubwa, mama yake na mawakili wake hadi katika ubalozi wa Tanzania nchini Kenya na baadaye kuelekea katika Wizara ya Mambo ya Nje mjini Nairobi, kuelezea hofu kubwa kuhusu hali ya mume wake akitaja kuwa hajazungumza naye tangu Jumatatu alipokamatwa.
"Alikuwa amekwenda kumjulia Agatha katika kituo cha polisi cha central kule Tanzania na akanipigia simu. Punde simu yake ikakatika na nadhani ni hapo ilipochukuliwa. Lakini si kawaida yake, angekuwa amefanya kila awezalo kupata njia ya kuwasiliana na mimi. Ila ni kimya tu. Kwa hivyo nina wasiwasi kwa sababu sijui kama hajiwezi, ameumia au yuko vipi," Alisema Njeri.
Njeri aliendelea kusema, "sio mara ya kwanza Boniface Mwangi kujipata katika changamoto za kisheria, ila familia yake inasema kwamba haijawahi kuwa kama ilivyo sasa anavyozuiliwa nje ya nchi."
"Ningependa kuiomba serikali ya Tanzania kumrejesha nyumbani na hata kama amekosa, tungependa afunguliwe mashtaka hapa nyumbani, manake nyumbani ni nyumbani. Watoto wana wasiwasi, wananiuliza kila siku alipo baba na sina majibu ya kuwapa. Hata kama atarudi akiwa hali gani, nitakubali, ila tu, namtaka mume wangu arejee nyumbani," Njeri alisema.
Mwanaharakati huyo alikuwa ameripotiwa kwamba ameachiliwa huru na kurejeshwa Kenya siku ya Jumanne, ila serikali ya Kenya ilithibitisha kwamba alikuwa bado anazuiliwa Tanzania.
Kenya na Tanzania ni nchi wanachama wa Mkataba wa Vienna wa 1963 wa Mahusiano ya Kibalozi, ambao unasema kwamba maafisa wa kibalozi watakuwa uhuru wa kuwasiliana na kuwafikia raia wa nchi iliyowatuma kuweza kuwafikia.
Aidha maafisa wa kibalozi wana haki ya kumtembelea raia wa taifa alikotoka wakati anapokuwa gerezani au kizuizini kuzungumza na kuwasiliana naye, na kupanga uwakilishi wake wa kisheria.
Yupo wapi Agatha Atuhaire?
Yupo wapi Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire? Haya yalikuwa maswali makubwa mawili kutoka kwa familia, raia wa Kenya na wanaharakati wa Tanzania, Kenya na Uganda, baada ya wanaharakati hao wawili kutorejea nchini mwao kama ilivyotarajiwa.
Mwangi alishikiliwa pamoja na mwenzake huyo kutoka Uganda Agatha Atuhaire. Mwangi imethitishwa kupatikana lakini bado swali linabadi yuko wapi Agatha Atuhire? haifahamiki alipo, Agatha mpaka sasa.
Kwa upande wa mwaMRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC),ameiambia BBC kwamba hawajapata taarifa ya alipo Agatha na wanaendelea kufuatilia
Wanaharakati hawa walishikiliwa na polisi mei 19 wakiwa hapa nchini ambako walifika kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili, Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu.
Rais Samia: "Tusiwe shamba la bibi" - aonya wanaharakati wa nchi jirani

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, wiki hii alitoa onyo kali kwa wanaharakati kutoka nchi jirani kuacha kuingilia masuala ya ndani ya Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo haliwezi kuwa "shamba la bibi" ambapo kila mtu anaingia na kufanya apendavyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 (Toleo la 2024), Rais Samia alisema kuna mwenendo unaoibuka wa baadhi ya wanaharakati kuvuka mipaka na kuingilia masuala ya ndani ya nchi, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa.
"Tusuiwe shamba la bibi kwamba kila mtu anaweza kuja na kusema anachokitaka… Tumeanza kuona mtitiriko au mwenendo wa wanaharakati ndani ya region (kanda) yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku," alisema Rais Samia.
Kauli hiyo aliitoa siku moja baada ya wakili mashuhuri wa Kenya na aliyewahi kuwa Waziri wa Sheria, Martha Karua, pamoja na Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga kuzuiwa kuingia nchini Tanzania.
Pia nao, walikuwa wamewasili kushuhudia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu, ambayo ilikuwa ifanyike katika Mahakama ya Kisutu.
"Sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika watu wako na usalama na amani na utulivu ni hapa kwetu, aliongeza Rais Samia.