Daktari anayesaidia wagonjwa kufa

Chanzo cha picha, Stefanie Green
Tahadhari: Ripoti hii ina maelezo ya wazi ya taratibu zinazopelekea kifo.
"Akiwa amelala kwenye varanda ya jengo la ghorofa. Ni mazingira mazuri, na marafiki wakiwa karibu naye. Ninakaribia kumdunga dawa, na anashika mikono yangu, ananitazama machoni, na kusema, 'Dkt. Green, hii kidogo itaonekana kuwa sio sawa, lakini nafkiri umeokoa maisha yangu. Asante sana.'"
"Wakati kama huo hauwezi kusahaulika," anasema daktari wa Canada Stefanie Green.
Lakini kinyume na inavyoonekana, dawa alizompa kwa njia ya mishipa na mgonjwa akitoa shukrani, hazikuwa tiba ya maumivu yasiyovumilika aliyokuwa akiyasikia.
Dawa hizo zilikuwa ni mchanganyiko wa vitu ambavyo vingemuua ndani ya dakika chache.
Stefanie Green ni miongoni mwa madaktari wa kwanza wanaosaidia watu kufa nchini Canada. Yeye pia ni mwandishi wa kitabu chake cha kumbukumbu kiitwacho "This is Assisted Dying," ambamo anasimulia uzoefu wake katika tasnia ya utabibu.
Tovuti yake inasema, kusaidiwa kufa sio kumaliza maisha ya mtu.
"Magonjwa na mateso ndio chanzo cha kugeukia chaguo hilo. Ninavyoelewa mimi, kusaidia kufa inaegemea zaidi kwenye kutimiza matakwa ya mtu."
Green ameolewa na msomi wa Kibrazili, ana watoto wawili, na anaishi Victoria, katika jimbo la Canada la British Columbia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchini Canada, sheria imeruhusu kusaidiwa kufa kwa karibu miaka kumi.
Mnamo mwaka wa 2016, nchi hiyo kwanza ilianzisha sheria inayoruhusu maombi ya kusaidiwa kufa kwa watu wazima walio na magonjwa yasiyotibika ambayo husababisha mateso yasiyovumilika au wagonjwa mahututi.
Mnamo mwaka 2021, kanuni zililegezwa ili kuruhusu wagonjwa wasio na magonjwa yasiotibika ambao wanaugua sana pia kusaidiwa kufa.
Na kuna mipango ya kuwezesha kusaidia kufa watu wazima walio na magonjwa ya akili pekee, bila hali zingine, ndani ya miaka miwili.
Green, mtaalam wa suala hili na aliyejitolea kwa miaka kusaidia wagonjwa wanaotaka kufa, anaakisi jambo ambalo linaweza kuonekana kama kinzani kwa wengi: wazo la daktari kusaidia wagonjwa kufa.
Green anatumia 75% ya wakati wake kusaidia watu kufa
"Watu wengi wanafikiri jukumu letu kama madaktari ni kuokoa maisha, na kwa kiasi fulani hiyo ni kweli. Lakini nadhani kiini cha kile ambacho daktari hufanya ni kuwasaidia watu," Green anasema.
"Tunasaidia watu kupambana na magonjwa, lakini mara nyingi hatuna chochote cha kuwasaidia nacho. Tunakumbana na magonjwa ambayo hatuwezi kukabiliana nayo na kufanikiwa. Na jukumu letu si kuwatelekeza wagonjwa," anaelezea BBC News Brasil.
"Ninaamini jukumu la daktari ni kusaidia watu katika hatua zote za maisha yao, na kusaidiwa kufa ni sehemu ya hilo."
Stefanie Green ana umri wa miaka 56. Alianza maisha yake ya kitaaluma akifanya kazi kama daktari mkuu na baadaye akajitolea kutunza wanawake wajawazito, kuwasaidia wakati wanajifungua, na watoto wachanga wanapozaliwa.
Baada ya zaidi ya miongo miwili katika tasnia hiyo, mnamo mwaka 2016, wakati sheria ya Canada ilipoanza kuruhusu raia kusaidiwa kufa, Green alibadilisha mwelekeo wake wa kazi.
Leo anatumia 75% ya wakati wake kusaidia watu kufa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Namna nilivyobadili mtazamo
Green anaeleza kwamba anaona kuna ufanano mkubwa kati ya ujuzi unaohitajika kwa madaktari na kusaidia mgonjwa kufa.
Kwake yeye, wakati wa kuzaliwa na kifo cha mtu, jukumu la daktari ni kuwa mwongozo katika mchakato wa asili.
Lakini alipoulizwa kwa nini alibadili mtazamo wake hadi kusaidia watu kufa, alitaja mambo kadhaa.
"Nilipinga sana wazo la kuacha kazi niliyokuwa nikifanya wakati nasaidia wanawake kujifungua," anasema. "Sikuweza kufikiria kitu kingine chochote ambacho kinaweza kunifurahisha kama hicho."
Hata hivyo, anasema kadiri miaka ilivyosonga, ilizidi kuwa vigumu kwake kijihisi sawa kutokana na zamu ndefu anapokuwa kazini akisaidia kina mama kujifungua.
Ilikuwa katika kipindi hiki ambapo Canada ilihalalisha kusaidia watu kufa. Green anasema alikuwa amefuatilia majadiliano kwa karibu mno.
"Kwa miaka 25 ya uzoefu wa kliniki, nimeona vifo vingi. Vifo vizuri, lakini pia vifo vibaya," anasema.
Siku chache baada ya sheria kuanza kutekelezwa, mgonjwa wa kwanza aligonga mlango wake. "Niko tayari, alisema."
"Mgonjwa wa kwanza"
"Bila shaka ilikuwa wakati wa kipekee. Ilikuwa kitu kisicho cha kawaida na hakika sitasahau wakati huo," anasema.
"Nina bahati sana na ninashukuru kufanya kazi na mgonjwa huyo na familia yake akiwa wa kwanza."
Anasema alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kusaidia watu kufa nchini Canada.
Harvey alikuwa mtu wa kipekee, anakumbuka. Alikuwa mgonjwa sana na kuna uwezekano mkubwa angekufa ndani ya wiki chache.
"Alikuwa mtu mwenye fikra za asili kabisa. Alikuwa akingojea tu mabadiliko ya sheria na yalipofanyika, akaja mlangoni kwangu akiwa na karatasi mkononi huku akisema, 'Hiki ndicho ninachotaka'."
Alikuwa anaungwa mkono na jamaa zake.
Harvey alilala kwa mara ya mwisho akitazama machoni mwa mkewe, ambaye alikuwa ameuoa kwa miaka 52.

Chanzo cha picha, Stefanie Green
Kusaidia watu kufa Canada
Vifo, kama kuzaliwa, ni hali za kipekee, anasema daktari. "Kwa sababu watu ni wa kipekee."
Lakini baada ya miaka mingi ya kufanya kazi hii, anasema kuna utaratibu ambao huwa anaufuata kwa wagonjwa wote.
Kabla ya kuelezea mchakato huo, Green anaelezea njia mbili zinazotumiwa nchini Canada kumsaidia mgonjwa kufa.
Njia ya kwanza ambayo ni nadra sana kutumika, daktari humpa mgonjwa dawa ya barbiturate yenye nguvu. Mgonjwa mwenyewe hunywa kioevu hicho na kulala usingizi, kisha hupoteza fahamu na kufa ndani ya nusu saa.
"Ile inayotumika na wengi, anaelezea, ni dawa ambayo daktari humdunga mgonjwa kwenye mshipa."
Dawa nne hutumiwa. Ya kwanza, ni dawa ya wasiwasi, hutumiwa kumfanya mgonjwa atulize akili yake.
"Ni kipimo cha juu na asilimia 98 au 99 ya wagonjwa hulala. Dalili zao hupotea, na kuhisi vizuri."
Dawa ya pili, ni ya hiari, ni kutia ganzi mshipa ambapo dawa itawekwa. Green anasema ni njia ambayo huwa anaitumia.
Dawa ya tatu inatumika kumlaza mtu wakati wa upasuaji. Ikiwekwa kwa kiwango cha juu, humfanya mgonjwa kupata usingizi mzito, kisha anapoteza fahamu kabisa.
Wakati hii inatokea, kupumua kwa kawaida hupungua na kuacha. Watu wengi hufa baada ya dawa ya tatu, lakini Green anasema madaktari hawategemei hio.
"Wana data nyingi za usalama, kwa hivyo, tunatumia dawa ya nne ambayo inasumbua harakati za misuli kwenye mwili.
"Kwa hiyo, natumia dawa hizi nne na ninajua zikidungwa kwenye mshipa wa mgonjwa atakufa," anasema.
"Hii ni njia ya kikatili ya kuielezea, lakini ndivyo inavyotokea."

Chanzo cha picha, Getty Images
"Wanalala na kufa"
Kifo cha mgonjwa ni mwisho wa mchakato mrefu ambapo Green hutathmini vigezo vitano ili kubaini kama mtu huyo anastahili kusaidiwa kufa chini ya sheria:
- Mgonjwa lazima awe na umri wa zaidi ya miaka 18.
- Lazima uwe na haki ya kupata huduma ya afya ya umma nchini Canada.
- Lazima utume ombi kwa hiari, bila kuingiliwa na wengine.
- Mgonjwa lazima awe sawa kiakili kuomba ombi hilo, ikimaanisha kuelewa ni nini kibaya kwao wenyewe na kuwa na uwezo wa kukubaliana na utaratibu.
- Mtu anapaswa pia kufahamishwa kuhusu chaguzi nyingine zinazopatikana ikiwa ni pamoja na huduma ya kupooza.
Sheria pia inamtaka mgonjwa awe na ugonjwa usioweza kutibika ambao amekuwa nao kwa muda. Mgonjwa lazima awe anateseka kwa njia ambayo inachukuliwa kuwa haiwezi kuvumilika na isiyokubalika.
"Pamoja na hayo yote, kuna taratibu kadhaa zinazohitaji maoni ya wataalam," anaongeza. "Na ikiwa mwisho wa mchakato huu sina uhakika mtu huyo anakidhi vigezo, sitasaini karatasi."
Siku iliyopangwa, daktari anafika mahali alipochaguliwa na mgonjwa kupokea huduma. Ikiwa mtu alichagua njia ya mishipa, daktari anaongozana na muuguzi.
"Ninatumia takriban dakika kumi peke yangu na mgonjwa na kutathmini tena kama hiki ndicho anachotaka. Daima ana fursa ya kubadilisha mawazo yake, hadi dakika ya mwisho."
Green anasema kwamba katika mazungumzo haya pia anatathmini hali ya akili ya mgonjwa. Je, unaweza kutoa idhini?
"Wanahitaji kujua mimi ni nani na kwa nini nipo pale. Ikiwa bado wanataka kusonga mbele, muuguzi anaingia na kumdunga mgonjwa sindano kwenye mkono."
Wakati huo huo, Green anazungumza na wageni wa mgonjwa. Kawaida ni jamaa wa karibu, wakati mwingine kunakuwa pia na marafiki, au mwenzi wa mgonjwa.
"Ninaeleza hatua kwa hatua kitakachotokea. Hili likishafanyika, tunakutana mahali ambapo mgonjwa amechagua. Inaweza kuwa sebule, bustani au chumba cha kulala."
"Tunatoa fursa kwa ibada yoyote ambayo mgonjwa ameomba. Maombi, kusoma bibilia, muziki. Wakati mwingine, mtu anataka kuzungumza, kusimulia hadithi, kucheka, kulia, au kusema kwaheri kwa mara ya mwisho. Wengine hawataki chochote, wengine wanataka mengi,"anaelezea.
"Namuuliza mgonjwa mara ya mwisho ikiwa anataka kuendelea na mchakato huo, akiruhusu, nachukua dawa na baada ya kumueleza mgonjwa ninachofanya ninaanza taratibu.
"Bila haraka, ninawapa dawa zao, na wanalala mbele ya familia yao. Kwa utulivu, kwa raha, kwa heshima. Wanalala na kufa."
"Wakati mwingine mimi hulia, mimi ni mwanadamu"

Chanzo cha picha, Getty Images
Green anaeleza kwamba anakuwa na mazoea ya kujulisha familia mgonjwa anapofariki.
"Wakati huo, mimi hutoka chumbani na kuwaacha wanafamilia peke yao ili waanze kuomboleza na kukaa kwa muda mfupi na mpendwa wao."
Green anasema kwamba kabla ya kuondoka, anazungumza na familia tena.
"Tunazungumza kilichotokea, wanashirikisha hisia zao. Tunapitia taratibu rasmi, tunaita hospitali ya kuhifadhi maiti," anafafanua.
"Mimi huwa nakaa kwa muda wa saa moja. Huo ndio utaratibu."
Tunapomuuliza ikiwa hutekwa na hisia, Green alikaa kimya kwa muda na kusema. "Oh, ndiyo. Hakuna mwanadamu ambaye hawezi kuguswa akiona mwingine akifa");